Mahakama ya Tanzania inakusudia kushirikiana na Australia ya Kusini katika teknolojia za kuendesha mashauri mahakamani ili kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa Haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Akizungumzia ziara ya Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini Mheshimiwa Christopher Kourakis iliyoanza leo nchini, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema ziara ya kiongozi huyo inalenga kuimarisha na kujenga ushirikiano katika maeneo matatu likiwemo eneo la teknolojia ya kuendesha mashauri mahakamani.
Alisema Australia ya kusini inaendesha mashauri mahakamani kwa kutumia teknolojia ya kisasa hivyo Mahakama ya Tanzania haina budi kuhama kutoka mifumo ya kuendesha mahakama kwa mkono kwenda kwenye teknolojia ya kidijiti
Alisema Mahakama inakusudia kuwapeleka wasajili na watendaji wa mahakama nchini Australia ya kusini ili wakajifunze mifumo hiyo kwa ajili ya kuanza kuitumia kuendeshea mahakama za Tanzania.
Aliyataja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni eneo la utoaji wa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu na Wasajili wa Mahakama ya Tanzania huku akisema eneo la tatu ni la namna ya kuanzisha Kada mpya ya Wapiga Chapa Maalum wa Mahakama watakaokuwa wakitumia mashine ndogo inayochapa wakati mashauri yakiendelea Mahakamani.
Akiielezea kada hiyo mpya, Jaji Mkuu alisema itawezesha kupatikana kwa nakala za mashauri ndani ya siku moja na kwamba watumishi hao ni tofauti na makatibu Muhtasi ambapo mishahara yao itakuwa ni mikubwa kuliko ile ya Makatibu Muhtasi.
Naye Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini alisema Mahakama za nchini kwake zinaendesha mashauri kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidijiti hivyo nchi yake itashirikiana na Tanzania ili nayo iweze kuendesha mashauri mahakamani kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akizungumzia kuhusu adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa kesi za mauaji nchini Australia ya Kusini, Mheshimiwa Kourakis alisema adhabu hiyo iliondolewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo msukumo wa Haki za Binadamu.
Alisema nchi yake pia ina mfumo ambapo endapo mtuhumiwa wa mauaji atakiri kosa ndani ya wiki sita basi atapunguziwa adhabu yake kwa asilimia 40. Aliongeza kuwa adhabu ya kifo nchini kwake ni kifungo cha maisha na endapo atakiri kosa atapunguziwa adhabu. Kiwango cha chini cha adhabu ya kifo ni kifungo cha miaka 20 jela.
Jaji Mkuu wa Australia ya Kusini leo ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini ambapo ametembelea Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu na pia anatarajia kutembelea Mahakama ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment