NA
NIHZRATH NTANI
NI wakati nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari pale Airwing, imepita miaka mingi sasa. Wakati huo nilikuwa bado ningali na umri wa utoto, bahati mbaya nikakikuta kitabu cha 'Kusadikika' hasa nilipofika kidato cha tatu.Nilikuwa mahiri sana wa kusoma vitabu darasani . Moja ya vitabu hivyo ni hiki kinachoitwa 'Kusadikika' ambacho kilikuwa kitabu cha kiada kwa wakati huo. Kitabu hiki kiliandikwa hata mimi sijazaliwa, bila shaka hata wewe umekikuta kitabu hiki, kiliandikwa nyakati za utawala wa Mwingereza. Kipindi hicho hakukuwa na Taifa la Tanzania wala ndoto ya kuwa kuna siku itakuja anzishwa Taifa la Tanzania. Sikukielewa hata kidogo kitabu hiki.
Miaka michache baadae nikakikuta tena kitabu hiki, pale nilipokuwa kidato cha tano. Huko sasa kilikuwa kitabu cha ziada, kwa mara nyingine tena sikuweza kumuelewa Shaaban Robert. Alitumia falsafa mgumu mno na kwa umri wangu wakati huo ilikuwa ngumu kumuelewa Shaaban Robert kwa kupitia kazi yake hiyo ya 'Kusadikika'. Umri wangu ukatimia na nyakati hazikuweza kurudi tena nyuma na kuyakumbuka yaliopita.Nimekuwa mtu mzima sasa.
Ni kama ambavyo nilishindwa kumuelewa Agape Fue kipindi kile cha uchaguzi wa TFF. Yuko wapi Agape Fue, Mwanadamu ambaye hakuna aliyemfahamu, hakuna aliyemsikia, hajulikani anapoishi, hakuna anayejua jinsia yake ama mwanamke au mwanaume hata jina lake hatuwezi kuliweka katika mizani ya jinsia.Pengine alikuwa mjumbe kutoka kuzimu akaja kutabiri haya tunayoyaona katika soka letu.Mjumbe huyu kutoka kuzimu alikuwa maarufu mnamo mwaka 2013 na jina lake lilikuwa maarufu sana katika pingamizi la Bwana mkubwa huyu wa TFF.
Katika watu wanaokaribia milioni hamsini katika Taifa linalopenda soka ni Agape Fue peke yake aliyaona haya, bahati kubwa hii ilioje?. Kaka yangu Angetile Osiah popote ulipo, tafadhali naomba unipatie namba ya Agape Fue angalau nimuone alivyo, mwanadamu mwenye bahati kubwa kama alivyo Shaaban Robert katika kuyafahamu yajayo.
Wapi soka letu linapoelekea? Ukitazama matendo na matukio yanayojiri kila siku katika soka letu ni kama matukio yale yaliomo ndani ya nchi ya Kusadikika.Wako wapi watu wa 'Gunness record' angalau waje hapa kuyachukua matukio yetu na kuyaweka katika kitabu hiki. Nina hakika ni Tanzania pekee matendo hayo yanapatikana. Ebu fikiria haya. Ni Tanzania pekee mchezaji na viongozi wa klabu hawajui muda wa mkataba waliosaini, malumbano yanaibuka mmoja anasema miwili, na mwingine mitatu hata wale waliopewa mamlaka ya kutunza mkataba huo nao hawajui ni miaka mingapi, ni ajabu kubwa hili?
Wakati unapoendelea kutafakari ni Tanzania peke yake kiongozi wa klabu anabishana na wasimamizi wa soka kuhusu kanuni ya adhabu ya mchezaji. Jambo hili huwezi kulipata popote zaidi ya hapa Tanzania. Endelea tu kushangaa ni Tanzania peke yake kocha bora huteuliwa kwa yule aliyeiepusha klabu kushuka daraja, sio yule aliye na mafanikio ya ubingwa. Bado naendelea kuwaza kumbe yule mholanzi Dick Advocaat kocha wa Sunderland aliyeiepusha timu yake kushuka daraja kumbe angekuwa hapa kwetu angetangazwa kuwa kocha bora mbele ya Jose Mourinho? Hapa naweza kumuelewa Malinzi pengine anataka kutupeleka katika mfumo wa peke yetu. Nani anajali?
Bado nabakia kushangaa, Kipa bora ni yule ambaye hakucheza mechi nyingi, alituhumiwa kwa utovu wa nidhamu, ni yule ambaye timu yake ilishika nafasi ya katikati ya ligi, yule ambaye aliyecheza mechi nyingi, aliyefungwa magoli machache, yule aliyeipa ubingwa timu yake hastahili kuwa kipa bora. Hakika upumzike kwa amani marehemu Shaaban Robert kwa kutabiri haya.
Wakati mwingine najiuliza, mchezaji bora wa ligi hawezi kuanza katika timu ya Taifa, pengine hili silijui hata lile la mchezaji ambaye hana nafasi katika klabu yake, huku akiwa hajaichezea klabu yake hata kwa asilimia 20 tu bado anastahili kuchaguliwa timu ya Taifa?.Wakati unaendelea kushangaa haya, basi kubwa lingine ni hili katibu wa zamani wa kamati ya uchaguzi wa klabu ambaye kamati hiyo ilivunjwa, bado anakuwa na mamlaka ya kuita waandishi wa habari na kutangaza tarehe ya uchaguzi. Nachoka kabisa.
Jiulize hili ni Tanzania pekee Rais wa Taasisi ya michezo anatoa mamlaka ya kuhamisha ofisi katika jengo linalomilikiwa na taasisi hiyo kisha wanaenda kupanga sehemu ya gharama kubwa, katika Taifa ambalo viwanja vya soka sio tu havifai kuchezea mpira bali hata kujifunzia mpira huo.Pengine pesa hizo zingetosha kukarabati sehemu ya kuchezea angalau kwa pato la mwaka mmoja. Hii ajabu kweli kweli.
Umeuona uwanja wetu wa Taifa ule mkubwa?, Kama wewe ni mgeni wa pale Chang'ombe ukienda leo unaweza kupigwa na butwaa, viwanja viwili vyenye hadhi sawa vimejengwa pamoja. Mpaka sasa bado sijaelewa vyote kujengwa pale. Hapo nikamkumbuka rafiki yangu mmoja raia wa Ujerumani aliyekuwa mwanafunzi wa lugha ya kiswahili pale Udsm, alipata niambia jambo hili, eti nchi yetu ni tajiri sana pia tumebalikiwa kuwa na vivutio vingi ajabu vya watalii kisha akacheka na kusema hata matendo ya watanzania pia ni sehemu ya utalii huo. Nikaduwaa! kisha sikumuelewa, sasa ndio namuelewa rafiki yangu huyu, lakini hayupo tena nchini natamani kumpigia simu na kumwambia sasa nimekuelewa.
Baada ya kutambua haya yote, mwisho ndipo nagundua nchi ile ambayo hayati Shaaban Robert aliizungumzia katika 'Kusadikika' ni nchi hii TANZANIA. Bahati nzuri kipindi hicho haikuwapo nchi inayoitwa Tanzania. Matendo ya soka letu ni yale aliyozungumza Shaaban Robert katika Kusadikika. Bila shaka gwiji huyu wa fasihi anastahili kupewa shahada ya heshima ya falsafa ya udaktari yaani PHD, natamani kuona jina lake lingeanzia na Dr Shaaban Robert lakini bahati mbaya Shaaban Robert si mwanasiasa kuweza kustahili heshima hiyo. Aibu ilioje?0713414189
No comments:
Post a Comment