• Breaking News

    Wednesday, 5 October 2016

    ZANZIBAR KUFANYA UTAFITI WA HALI YA UZALISHAJI WA MAYAI


    Na Masanja Mabula –Pemba
    WIZARA ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi Pemba inatarajia kufanya utafiti wa hali ya uzalishaji wa mayai pamoja na kutambua mahitaji ya soko kabla ya kushawishi hoteli za kitalii na makampuni mengine kuingia mkataba wa kununua mayai ya wafugaji kisiwani hapa.
    Afisa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo Pemba Asha Zaharani  amesema kuwa uwamuzi wa kufanya utafiti huo umekuja baada ya kubaini kuwepo na mrundikano wa mayai kwa wafugaji wa kuku   ambayo yamekosa wateja .
    Akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Wete , wakati wa ziara ya kuwatembelea wafugaji wa Kuku katika Shehia ya Kisiwani kwa Binti Abeid Wilayani hapa , amesema Idara inatambua kuwepo na changamoto ya  soko la kuuzia mayai kufuatia kuongezeka kwa uzalishaji wa mayai kwa wajasiriamali hao .
    “Katika kukabiliana na changamoto ya soko , Idara imejipanga kufanya utafiti kwa lengo la kubaini hali ya uzalishaji pamoja na mahitaji ya soko la ndani  jambo ambalo litaiwezesha Idara kufanya ushawishi wa kampuni kuingia mkataba wa kununua bidhaa ya mayai ”alieleza.Mapema wafugaji wa kuku katika shehia hiyo walilalamika kukosa soko la kuuzia mayai na kusema kwamba zaidi ya trea elfu moja za mayai (1000) yanayozalishwa na wafugaji wa Kisiwani kwa Binti Abeid  yamekosa soko .
    Mmoja wa wafugaji hao Mussa Hamad Mussa akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake alimwambia Mkuu wa Wilaya kuwa ukosefu wa soko umepelekea pia mifugo yao kuathirika na maradhi na njaa kutokana na wafugaja kukosa fedha za kununulia mahitaji hayo .
    Naye Afisa  Biashara Kutoka Wizara ya Biashara , Viwanda na Masoko Pemba Ali Suleiman aliwashauri wafugaji hao kuuanzisha mtandao wa wafugaji wa Kuku Pemba ili wawe na sauti moja na itarahisha kupatikana soko la uhakika .
    Alisema mtandao huo utakuwa kiunganishi cha wafugaji wa kuku Kisiwani Pemba , kwani wateja wanaohitaji mayai watawasiliana na uongozi wa mtandao ili kupata mahitaji na idadi  ya mayai wanayohitaji  .Katika nasaha zake Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid amesema kwamba Serikali ya Wilaya imeunda kikosi kazi ambacho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha mayai yote yanayozalishwa na wafugaji hao kila siku na wajasiriamali hao yanauzwa .
    Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wafugaji hao wa kuku kutovunjika moyo bali waendelee na kazi ya kuzalisha mayai kwa wingi na kwani Serikali inathamini juhudi na mchango wa wafugaji hao wa katika mapambano dhidi ya adui maskini .
    “Katika kuthamini mchango wa wafugaji hao, serikali imeunda kikosi kazi ambacho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba mayai yote yanayozalishwa kila siku yanapata soko ”alisisitiza.
    Afisa Kutoka Mradi wa kumuwezesha mwanamke , Omar Mtarika Msellem aliahidi kwamba mayai hayo zaidi ya trea elfu moja yanakuwa yamenunuliwa ndani ya kipindi cha siku tatu , ambapo atakuwatana na wa wafanyabiashara wa  mayai wa ndani ili kuwashawishi  kuyanunua .
    Hata hivyo Mtarika alielezea kuridhishwa na hali ya uzalishaji wa mayai kwani umevuka lengo lililotarajiwa kutokana na wafugaji kunufaika na elimu inayotolewa na asasi za Serikali na binafsi ndani na nje ya Kisiwa cha Pemba.
    Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Maendeleo na Mifugo Pemba ni kwamba jumla ya trea elfu nane za mayai huzalishwa kila siku Kisiwani Pemba huku trea elfu nne kila siku  huzalishwa katika  Wilaya ya Wete

    No comments:

    Post a Comment