WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amekiri kuwapo na ugumu wa kufanya siasa nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujitoa na kufanya kazi kwa moyo.
Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitoa kauli hiyo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani jana wakati wa shughuli ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Chadema iliyopo wilayani humo.
Alisema wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya chini wanapaswa kujitoa katika shughuli za ujenzi wa chama ili kuweza kufikia lengo la kushika dola ifikapo mwaka 2020.
“Ninaamini wote tuliopo tutajitoa kwa moyo mmoja, najua ni kazi ngumu kuwa na chama tofauti na chama tawala lakini tunapaswa kupambana kufikia malengo,” alisema.
Sumaye ambaye kabla ya kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana hazijaanza alijitoa CCM na kuhamia Chadema kwenda kumwongezea nguvu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alisema kwa sasa hata CCM inajua kuwa Chadema itashika dola hivyo vijana wakijenge kuanzia ngazi ya matawi.
“Lazima tujitolee, dola haipatikani kiurahisi, tunapaswa tuwaeleze wananchi tutawafanyia nini, hatuwezi kufanya kazi za chama kwenye nyumba ya mtu au ofisi za vichochoroni kuanzia mwaka 1992,” alisema Sumaye.
Naye Katibu Mkuu Taifa wa Chadema, Vicent Mashinji, alisema kwa sasa ni wakati wa kudai Katiba Pendekezwa iliyokuwa ikisimamiwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, ili kupunguza madaraka ya rais.
“Tunahitaji Katiba ya wananchi, tunapaswa kufanya hii kampeni kwa ngazi ya msingi, tunahitaji rais hatuitaji Mungu, rais asiseme mimi sichezewi kwa sababu yeye si Mungu, ambaye hachezewi ni Mungu tu binadamu wote kuna aina ya kuchezeana,” alisema Mashinji.
Pia alisema Katiba mpya itasaidia kupata tume huru ya uchaguzi huku akirejea uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar Machi 21, mwaka huu na kudai kuwa Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kukurupuka bila kufuata sheria za nchi.
“Siamini kama miaka yote tutavumilia, uvumilivu una kikomo, tunalalamika lakini inawezekana safari ijayo wakalalamika wao, kila siku mnasema hatushindi tutashinda tu,” alisema Mashinji.
Alisema kwa mwenendo wa Serikali iliyopo bila Katiba mpya nchi inaweza ikaingia katika machafuko bila sababu za msingi.
Mashinji alisema Taifa linabomoka kuanzia juu kwenda chini na itakuwa ngumu kuliokoa.
Alisema katika uongozi demokrasia ni suala la msingi na si kuongoza nchi kwa matamko na amri.
Katika hafla hiyo, jumla ya Sh milioni 9.9 zilipatikana ikiwamo ahadi na kati ya hizo Sh milioni tatu zilitolewa na Dk. Mashinji.
No comments:
Post a Comment