Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) cha mkoani Arusha, Allan Mbando, ameibwaga Serikali katika kesi ya kudaiwa kusambaza ujumbe kupitia Mtandao wa Facebook akimtaka Mwamunyange apindue nchi.
Katika mtandao huo wa kijamii, Mbando, anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka kwamba: “Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje, halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti.”
Kutokana na madai hayo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilimfungulia mashtaka Mbando ya kudaiwa kusambaza ujumbe huo uliokusudia kueneza na kufanya uchochezi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo mjini hapa juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Augustine Rwizile, alisema mahakama hiyo imepitia kwa kina hoja na ushahidi wa pande zote mbili katika kesi hiyo.
Hakimu Rwizile alisema baada ya kupitia ushahidi katika kesi hiyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo haukuweza kuwasilisha ushahidi unaoweza kumtia hatiani mshtakiwa.
Alisema mbali na ushahidi huo kutojitosheleza, pia hapakuwapo na jambo lolote lenye nia ovu ya kusababisha au kufanya uchochezi katika ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa.
“Sasa mahakama hii inamwachia huru mshtakiwa baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yake pasipo kuacha shaka yoyote.
“Lakini pia kama kutakuwa na upande ambao haujaridhika katika hukumu hii unaweza kukata rufaa,” alisema Rwizile.
Akisoma hukumu hiyo, alisema ujumbe uliosambazwa haukuwa na umuhimu wowote kwa kuwa haukumwelezea Mwamunyange ni nani katika nchi anayotakiwa kuipindua huku pia ujumbe huo ukiwa haukutaja nchi iliyolengwa kupinduliwa.
“Ujumbe ulioandikwa katika Facebook haumtambulishi Mwamunyange ni nani. Lakini ujumbe hauonyeshi jambo la msingi lenye uhusiano wa kisiasa katika Taifa linalodaiwa,” alisema Rwizile.
Kutokana na sababu hizo ikiwamo ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo kushindwa kuthibitisha ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa, mahakama ililazimika kumwachia mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo katika kesi hiyo alikuwa akitetewa na Wakili Moses Mahuna.
Mbando anaongeza idadi ya watu walioshtakiwa mahakamani kutokana na makosa ya mtandaoni baada ya Aprili, mwaka huu mkazi mwingine wa Arusha, Isack Habakuki (40), kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kusambaza lugha ya matusi na dhihaka kwa Rais Dk. John Magufuli.
Baada ya kesi hiyo kuendelea kusomwa mahakamani hapo, Isack alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni saba na yeye alikubali kuzilipa kwa awamu.
Mtu mwingine aliyeshtakiwa Aprili, mwaka huu kwa makosa ya mtandaoni ni kondakta wa daladala, Hamimu Seif (42), aliyepandishwa kizimbani kwa kosa analodaiwa kulifanya Machi 10, mwaka huu alipotishia kumuua Rais Magufuli kwa maneno akiwa katika Baa ya Soweto iliyopo Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment