• Breaking News

    Friday, 7 October 2016

    Simba yamwomba msamaha Rais Magufuli kwa mashabiki wake kuvunja viti vya Uwanja wa Taifa


    Baada ya kujitokeza tukio la mashabiki wa Simba kuvunja viti vya Uwanja wa Taifa katika mchezo wa Yanga na Simba kisha Rais John Magufuli kuelezea masikitiko yake kwa kile kilichojitokeza katika mchezo huo, klabu ya Simba imejitokeza na kumuomba rais msamaha.

    Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Simba, Haji Manara amesema klabu inakubali kufanya kosa hilo na kwa pamoja kuanzia rais hadi mashabiki wanaomba msamaha kwa Rais Magufuli na kuahidi jambo hilo halitajitokeza tena.

    “Rais wa klabu ya Simba, kamati ya utendaji, sekretarieti, benchi la ufundi na wachezaji, wanachama na mashabiki wa Simba wanaomba radhi kwa Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kupitia kwa waziri mwenye dhamana ya michezo, Nape Nnauye kwa kitendo kisicho cha kiungwana kilichofanywa na mashabiki wetu katika mchezo wa Yanga,

    “Tumeona twende mbali na tumwombe radhi rais wetu, hizi ni rasirimali zetu, zinajengwa na kodi zetu, serikali inatumia gharama  kubwa kuziendeleza rasirimali hizi, ni upuuzi wa hali ya juu kabisa kufanyika kitendo kama kile,” alisema Manara.

    Aidha Manara amesema klabu ya Simba inaamini serikali itawaruhusu tena kuendelea kutumia uwanja wa taifa na kwa wanachama wote ambao watabainika kufanya uharibifu ule watachukuliwa hatua za kisheria.

    “Tunaamini serikali itarudi nyuma na kuturuhusu kutumia uwanja wa taifa na katika hili tunaahidi tukio kama lile halitajitokeza tena, na kama klabu itabaini kuwa kuna wanachama wetu walishiriki kufanya tukio lile watachukuliwa hatua,

    “Na tunaiomba serikali ifunge zile kamera za CCTV pale uwanjani ili tukio kama lile likijitokeza iwe rahisi kuwabaini waharifu waliohusika, ule ni uharifu wa makusudi, leo klabu inapata hasara, tunahangaika kufanya vikao mara wizara mara shirikisho kwa ajili ya watu wachache,” alisema Manara.

    No comments:

    Post a Comment