Katibu wa chama cha walimu mkoani Pwani, (CWT),Nehemiah Joseph ,akizungumza kuhusiana na wizi uliotokea katika jengo la chama hicho ,ambapo computer za mezani na mpakato 11 zimeibiwa na zaidi ya mil.5 .(picha na Mwamvua Mwinyi).
………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
OFISI sita zilizopo jengo la chama cha walimu mkoani Pwani(CWT)zimevunjwa na kuibiwa Kompyuta za mezani na mpakato 11 zinazodaiwa kufikia sh.mil 15 na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Mbali ya kuibiwa vitendea kazi hivyo,watu hao pia wamechukua kiasi cha fedha taslimu sh. mil 5,036,515 zilizokuwepo katika baadhi ya ofisi hizo.
Kufuatia tukio hilo, jeshi la polisi mkoani Pwani,linawashikilia walinzi wawili wa jengo hilo kutoka kampuni ya Noble security Tanzania ltd ya Kibaha,Hamad Kisoki(32)mkazi wa Mailmoja na Said Mohammed (39) mkazi wa Mwanalugali.
Akizungumzia kuhusiana na tukio hilo,katibu wa CWT mkoani humo,mwl Nehemiah Joseph,alisema tukio limetokea usiku wa octoba mosi kuamkia octoba 2 mwaka huu.
Alisema siku ya tukio walinzi waliotakiwa kuingia kazini walikuwa ni wawili lakini badala yake aliingia mmoja ambae ni Said Mohammed .
“Ambapo alipokuwa kwenye lindo anadaiwa kupatiwa chips na kinywaji aina ya juise vinavyosemekana kuwa na madawa ya kulevya kutoka kwa mwanamke asiyefahamika”.alisema.
Mwl.Joseph alielezea kuwa ,baada ya kupatiwa chakula hicho mlinzi alipoteza fahamu na hivyo kutoa mwanya kwa watu hao walivunja milango ya ofisi hizo na kuingia bila bughudha .
Alisema inadaiwa mwanamke aliyempatia chakula aliihitaji kuwapa chakula walinzi hao wote wawili kabla Mohammed hajaachiwa lindi lakini mwenzie Hamad alikataa na kusema anaenda kula nyumbani.
Mwl.Joseph alisema mwanamke huyo kwa hali ya kawaida atakuwa ni mmoja kati ya watu hao kwani haiwezekani ampatie mtu chakula kisha apate madhara na kutokea wizi huo.
Alizitaja ofisi zilizopo kwenye jengo la CWT mkoa ambazo zimeibiwa ni pamoja na CWT mkoa computer 1 na fedha sh.mil 1.532,CWT wilaya computer 2 na mil moja,beem financial services (BFS) computer moja na mpakato(laptop) moja.
Ofisi nyingine ni Chodawu computer 2 na mpakato moja,Tuico computer 1 na mpakato moja pamoja na fedha ,mil.1.170 na TCCIA iliyoibiwa computer moja na fedha mil.1,334,515.
Katibu huyo wa CWT mkoani hapo,alieleza kwasasa wameshafikisha taarifa hizo jeshi la polisi wilaya na mkoa kwa hatua zaidi na ofisi ya chama hicho imeshakaa na taasisi zote zilizopanga jengo hilo kufanya tathmini.
Mwl.Joseph alisema kampuni ya Noble Security waliingia nayo mkataba hivyo baada ya kufanyika tathmini wataipatia ili kuangalia namna ya kulipia gharama zilizotokea.
“Inasikitisha sana kutokea kwa wizi huu lakini kwa hili iwe fundisho kwa walinzi wengine,waache kula kula ama kununua vyakula kwa watu wasiowajua,kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha kuwapa upenyo wahalifu na kuletea hasara kwa wenye mali”alisema mwl Joseph.
Kwa upande wake,kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi ,alikiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia octoba 2 (jumapili).
Mushongi alisema majira ya saa 5 asubuhi walipata taarifa za kuvunjwa kwa jengo hilo kutoka kwa Elizabeth Thomas ambae ni katibu wa chama hicho wilaya ya Kibaha huko mkoani A ,kata ya Tumbi.
Hata hivyo ,Kamanda huyo alisema ,baada ya kufanya wizi huo watu hao walitokomea kusikojulikana na jeshi hilo bado linawatafuta,huku akiomba ushirikiano kwa jamii kuwafichua watu wanaowadhania kuhusika na wizi huo.
Alisema kwasasa wanawashikili walinzi wawili kati ya walinzi wanaolinda jengo hilo kwa ajili ya uchunguzi juu ya wizi uliotokea.
Mushongi aliwaasa walinzi na wafanyakazi katika maofisi na taasisi mbalimbali mkoani humo,kuacha tabia ya kununua vyakula ama kupewa vyakula na mtu au watu wasiowajua ili kuepukana na madhara yoyote ikiwemo kuwekewa madawa ya kulevya .
No comments:
Post a Comment