• Breaking News

    Thursday, 1 September 2016

    Magufuli: Wanaolia njaa ni wapiga ‘dili



    RAIS John Magufuli amesema watu wanaolalamika kwamba fedha hazionekani mitaani ni watu waliozoea ‘kupiga dili’ (kujipatia fedha isivyo halali).
    Ameeleza kuwa wapo wananchi walioficha fedha ili wasibainike kuwa na kiwango kikubwa na kuwataka wazitoe, vinginevyo anaweza kuchapisha noti mpya na hizo zilizofichwa zikaoza.
    Akifungua Mkutano wa 14 wa Siku ya Wahandisi nchini uliofanyika Dar es Salaam jana, Dk Magufuli alioneshwa kukerwa na tabia ya watu waliozoea, kuifanya nchi kama shamba la bibi kwa kutapanya mali za umma huku baadhi ya watendaji wakikiuka maadili ya uongozi kwa maslahi binafsi.
    “Tanzania imechoka kuibiwa na kuchezewa kwa sababu kila mahali ni dili, ukigeuka huko wanapiga dili, huku ni dili, serikali kupitia mashirika ya umma mbalimbali ilikuwa haipati hela kwa sababu ya dili, ni dili tu kila mahali, sasa kwa mwendo huu wa kwangu hizo dili basi,” alisisitiza Rais Magufuli.
    Akizungumzia wananchi walioficha fedha, Rais Magufuli aliwataka wazitoe fedha hizo na ziende kwenye mzunguko wa fedha na kwenye miradi ya maendeleo, na kusisitiza kuwa anaweza kuamua kubadilisha noti na hizo zilizofichwa zikawaozea kwenye magodoro.
    Alisema wapo watu walioficha fedha na hali hiyo ilitokana na wao kuogopa kuulizwa wametoa wapi kiwango kikubwa cha fedha, hivyo waliamua kwenda kwenye benki walikohifadhi na kuzihamisha.
    “Awali wapo watu walioamua kuzihamisha hela kwenye benki na kuzificha, niliwaza sijui nichapishe noti mpya kusudi walioficha zikawaozee, kwa sababu nafahamu watu walikuwa na tabia ya kuhamisha fedha kutoka kwenye benki kwenda kuzificha, waliogopa wataulizwa wamezitoa wapi hela zote hizo,” alisema Rais Magufuli.
    Akisisitiza hilo, Rais Magufuli alisema ni vyema walioficha, wakazitoe na kuziingiza kwenye mzunguko zifanye kazi au wakiendelea kuzificha, atabadilisha noti na hizo zilizofichwa kwenye magodoro watajua watakapozipeleka.
    Akizungumzia suala la watu kulalamika kuwa fedha hazionekani mtaani, Rais Magufuli alisema watu wanaolalamika kwamba fedha hazionekani ni wale waliozoea kupiga dili na kwamba fedha hizo zilizosambaa mitaani, zilikuwa za watumishi hewa na kuanzia sasa hazitaonekana.
    “Msipofanya kazi hamtaona pesa, zimepotea kwa sababu tumebaini hela zilikuwa ni zile wa watumishi hewa na wapiga dili tumewatumbua na nitaendelea kuwatumbua iwapo nitabaini ulikuwa unapiga dili, ni lazima mfanye kazi mlipwe stahiki yenu na sio kupiga dili,” alisema.
    Alisisitiza kuwa wale waliozoea kupata fedha za bure, watambue kwamba jambo hilo halipo katika Serikali ya Awamu ya Tano, aidha waliokuwa wanafanya ‘misheni’ kwenye wizara mbalimbali nao watambue hakuna mchezo huo.
    Hivyo aliwataka wananchi na Watanzania kwa ujumla kufahamu kuwa hakuna fedha za bure, na zilizokuwepo kwenye mzunguko zimeondolewa jambo ambalo limesaidia kuimarisha thamani ya fedha ya nchi.
    Akisisitiza hilo alitoa mfano na kusema anakumbuka akiwa Geita, mfuko wa saruji ulikuwa unauzwa Sh 26,000 lakini hivi leo mfuko huo unauzwa Sh 16,000 jambo ambalo ni wazi kwamba thamani ya fedha ya Tanzania imeanza kuimarika kwa kuondolewa fedha chafu kwenye mzunguko.
    Hata hivyo, aliwaonya Watanzania waliozoea vya bure kwamba huu sio wakati wa kupata vya bure, bali watu watapata fedha kwa kufanya kazi na kuwataka wahandisi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia weledi ili kusaidia nchi kufika kwenye malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
    Katika mkutano huo na wahandisi zaidi ya 2,500, Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kusema pamoja na jitihada za serikali za kununua ndege mpya mbili, baadhi ya watu wanaziponda ilihali hawana hoja za kitaalamu.
    “Tumenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q 400 na zitaingia nchini Septemba 19, mwaka huu zikitokea Canada, na kwa nini tumenunua ndege hizo wataalamu mnajua ila wasio wataalamu hawajui na ndio wanaoziponda,” alisema Rais Magufuli na kufafanua kuwa zimenunuliwa kutokana na hali halisi ya viwanja vya ndege vilivyopo nchini na kwamba zina mwendo kasi zaidi na pia zinatumia mafuta kidogo ukilinganisha na ndege aina ya Jet.
    Katika hilo, Rais Magufuli alisema makandarasi wa ndani, wanapaswa kujitathmini kuona wana mchango gani katika kuendeleza nchi na kwamba hata katika ujio wa ndege hizo ni vyema wakaona wanawezaje kuzitunza kwa kutoa mchango wao kwenye matengenezo ya ndege na wasitumie nafasi kama hizo kujinufaisha.
    “Mfano tu juzi hapa waziri alimtumbua Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL), eti matengenezo ya kiwanja cha ndege cha Mwanza ya urefu wa nusu kilometa gharama yake ni bilioni 1.5, na kile kiwanja cha Dar eti nacho upanuzi wa njia ya kurukia na maegesho yamegharimu bilioni 650, gharama hizo ni kubwa sana na wakati mwingine wanaofanya hivyo ni watendaji tunaowaamini, nimesema kwa hili lazima uchunguzi ufanywe kwa kina,” alisema Rais Magufuli ambaye pia alirejea kauli yake ya kuumizwa kuona mchanga wa madini kupelekwa nje kwenda kuchunguzwa kama kuna madini au la ilihali nchini wapo wahandisi wa madini.
    Alisema katika uongozi wake, amejitahidi kila sekta ameweka mtaalamu mhandisi, akifahamu kuwa atakuwa kiungo muhimu katika kusukuma maendeleo. Alisema anatambua mchango wao katika ukuaji wa uchumi, lakini iwapo hawatajituma, nchi haitaendelea.
    “Nawaomba sana wahandisi mkiamua nchi ifike uchumi wa kati tutafika, na msipoamua hatutafika, nchi bila wahandisi haitaenda, sasa ni jukumu lenu kuangalia mnasaidiaje nchi, kwenye ujenzi wa reli je nafasi yenu ni ipi, bomba la mafuta nalo, mmejipangaje?” Alihoji Rais Magufuli.
    Siku ya Wahandisi sambamba na mkutano huo wa wahandisi umeandaliwa na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), na zaidi ya washiriki 2,500 wamehudhuria mkutano huo wa siku mbili unaomalizika leo ambao mada mbalimbali zinajadiliwa kuangalia nafasi ya wanataaluma hao katika kuiletea nchi maendeleo.
    Katika hatua nyingine, Rais Magufuli leo anatarajiwa kuzungumza na wananchi wa kisiwa cha Pemba kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale mjini Chake Chake.
    Aidha, anatarajiwa kuzuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Saba wa Tanzania, Dk Omar Ali Juma aliyefariki dunia Julai 4, 2001.
    Kesho Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Zanzibar kwa kuhutubia wananchi wa kisiwa cha Unguja kwenye Uwanja wa Kibandamaiti, ambako asubuhi anatarajiwa kwenda kutoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi aliyefariki mwezi uliopita

    No comments:

    Post a Comment