• Breaking News

    Thursday, 1 September 2016

    Japan yaombwa kusaidia kuzuia ujangili nchini



    WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameiomba Serikali ya Japan kuingilia kati suala la ujangili unaofanywa na baadhi ya raia wa nchi kadhaa duniani ikiwemo China kwa kuwa na soko la meno ya tembo linalosababisha kuuawa kila wakati kwa wanyama hao.
    Alisema kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Japan na China, wanaweza kuzungumza nao ili waone aibu kufanya ujangili katika maliasili zilizopo nchini.
    Profesa Maghembe aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na Rais wa Chama cha Uchumi na Maendeleo ya Afrika (AFRECO), Tetsuro Yano, aliyefuatana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida.
    Alisema nchi zenye masoko ya meno ya tembo ndio washiriki wakubwa wa ujangili. Aliongeza kuwa watakapohamasishwa na kuelimishwa kwa ajili ya kuvunja masoko yao, ujangili utapungua.
    “Ujangili ni moja ya changamoto kubwa inayolikabili taifa letu. Tunaiomba Serikali yako ya Japan izungumze na majirani zenu China ili waone aibu kufanya ujangili na kuuza meno ya tembo,’’ alisema Profesa Maghembe na kuongeza kuwa maliasili na utalii vinachangia katika kukuza pato la taifa.
    Alisema kutokana na hali hiyo, anaiomba Japan isaidie kamera kubwa itakayosaidia kuwawezesha kuwatambua majangili, meno na maeneo watakayokuwa wakiendesha ujangili. Alieleza kuwa vifaa vilivyopo havitoshi kuona matukio mbalimbali yanayofanyika katika hifadhi za taifa.

    No comments:

    Post a Comment