• Breaking News

    Wednesday, 31 August 2016

    Wabunge:Tumeibiwa, tumedhalilishwa



    MJADALA kuhusu wizi wa mtandaoni, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikiwemo matusi na udhalilishaji, vilitawala kwenye kamati ya bunge baada ya wajumbe wengi kutoa ushuhuda walivyoibiwa na wengine kudhalilishwa.
    Wameyasema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipokutana na viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) mjini Dodoma.
    Miongoni mwa wabunge ‘waliolia ’ kuhusu kudhalilishwa mtandaoni na kutukanwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM) aliyelalamika akisema licha ya kufanyiwa vitendo hivyo (bila kutaja ni nini), hakusaidiwa na mamlaka.
    “Watu wanadhalilishwa, wananyanyasika...kwa mfano mimi mwezi Aprili nilifanyiwa vitendo vibaya kwenye mtandao,” amesema na kulalamika kuwa watu wa kawaida wakilalamika hawasaidiwi, lakini viongozi wa juu wakifanyiwa vitendo hivyo, hatua zinachukuliwa haraka.
    Malalamiko kuhusu mbunge huyo, yalisababisha wabunge wengine kumzungumzia wakitaka asaidiwe kubaini wahusika. Hata hivyo, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), alisema,
    “Teknolojia ndiyo inaamua maisha...utegemee kipindi cha mapigo makubwa...kitu cha kwanza uwe na kifua kikuu.”
    Kuhusu wizi na utapeli kupitia simu za mkononi, ikiachwa wabunge wengi walioshuhudia namna walivyoibiwa, pia Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba aliwavunja mbavu aliposema pia yeye nusura atapeliwe kwa mtindo wa kupokea ujumbe wa simu ukitaka amtumie mtoto wake fedha.
    Wakielezea mtindo wa wizi ambao simu ya laini huzimwa kwa dakika chache na kisha namba zake kutumika kutuma ujumbe wa kuomba fedha, Mbunge wa Fuoni, Abbas Ali Mwinyi (CCM), alisema aliibiwa Sh 800,000 baada ya mtu aliyetumia namba ya ndugu yake, Dk Hussein Mwinyi kumuomba fedha hizo.
    Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM) amesema mfanyakazi wake ambaye ni meneja aliyeko kituo cha mabasi Ubungo, alitapeliwa Sh milioni 1.6 kwa njia hiyo ya simu.
    Mbunge wa Nanyumbu, William Dua (CCM) amesema, pia alinusurika kutuma Sh milioni moja baada ya kupokea ujumbe kutoka namba ya simu ya Mkuu wa Wilaya yake ukimuomba kiasi hicho cha fedha.
    “Nilipopiga akakata, nikaamua kumtuma mtu apeleke fedha taslimu, DC akashangaa...,” amesema.
    Akishutumu usajili holela wa laini za simu kuwa unachangia matatizo hayo ya wizi, utapeli na matusi, Mbunge wa Igulula, Musa Ntimizi (CCM) ameitaka TCRA ifanye uratibu wa mitandaoni kudhibiti watu wanaotuma picha chafu, wanaotukana na kudhalilisha wengine.
    Akielezea wizi huo ambao wahusika humnyang’anya mtu mtandao kwa muda, Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Kilaba alisema ulianza kuibuka Septemba mwaka jana.
    Amesema, mamlaka iliita kampuni za simu na kuzilazimisha kuwa na mfumo maalumu wa kudhibiti vitendo hivyo kwenye mitandao yao.
    Hata hivyo, alisema ingawa Machi ilionekana matukio hayo kushuka, bado wanaojihusisha na wizi huo wanakuwa wakibuni mbinu mbalimbali kupitia teknolojia.
    Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy amehimiza waathirika wa vitendo hivyo kuripoti polisi kwa kuwa wana mamlaka kisheria kuwashitaki wahusika.
    Hata hivyo alisema wanaendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa matumizi mazuri ya mitandao

    No comments:

    Post a Comment