Meneja wa Taasisi inayopiga vita maambukizi dhidi ya maradhi ya ukimwi Tanzania (TPHS) Frida Godfrey akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Malik Juma Akili msaada wa vifaa vya kutendea kazi kwa ajili ya matumizi ya wadau wa afya kwa lengo la kuongeza ufanisi.
……………………………………………….
Taasisi inayopiga vita maambukizi dhidi ya maradhi ya ukimwi Tanzania (TPHS) imeikabidhi Wizara ya Afya msaada wa vifaa vya kutendea kazi kwa ajili ya matumizi ya wadau wa afya kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Vifaa vilivyokabidhiwa vikiwa na thamani ya sh. milioni 27,820,000 ni pamoja na komputa 10, Printer saba na UPS.
Akikabidhi msaada huo Meneja wa Taasisi hiyo Frida Godfrey Radegunda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, amesema lengo ni kuimarisha vitendea kazi katika kutoa huduma bora za Afya kwa jamii.
Amesema Taasisi hiyo kwa kushirikana na Wizara ya Afya itaendelea kutoa huduma na kuwawezesha wananchi kuelewa njia za kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi ya ukimwi
“Taasisi yetu inashirikiana na wizara ya Afya kupambana na madawa ya kulevya katika vituo vya afya na kutoa elimu ya ukimwi na madhara ya kujidunga sindano, ” amefahamisha Meneja huyo.
Aidha amewataka wadau wa Afya kuvitumia vyema vifaa hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Malik Juma Akili ameishukuru Taassisi ya TPHS kwa msaada huo pamoja na kuisaidia kutoa elimu kwa jamii dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.
Amesema vijana wengi wanaathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kupelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la maambukizi ya ukimwi kwa kujidunga sindano ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Vijana wasikilize yale wanayoelekezwa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi kiwango cha maambukizi ni kikubwa Unguja ni asilimia 1.2 na Pemba ni 0.3 tusjiachie tujitahidi katika kupunguza,” alisisitiza Dkt. Malik.
Aidha Katibu Mkuu ameishukuru Taasisis hiyo kwa kufanikiwa kuifanyia matengezo Maabara kuu ya Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa lengo la kuboresha huduma kwa jamii pamoja na kukisaidia kituo cha huduma ya kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kupata nafuu (Methodone Clinic ).
Mapema Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad amesema kitengo cha Mfamasia Mkuu kilikuwa na upungufu wa vitendea kazi lakini msaada huo utasaidia kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa Tume ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bohari Kuu ya dawa pamoja na Hospitali ya Mnazi Mmoja.
No comments:
Post a Comment