• Breaking News

    Friday, 30 September 2016

    WATANZANIA WAASWA KUEPUKA VYAKULA VISIVYO BORA

    0003
    Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi
    ………………………………………………………..
    IMEBAINIKA kuwa ulaji wa vyakula visivyo bora husababisha maradhi ya magonjwa ya moyo kwa watu wazima wa miaka 45 hadi 60
    Aidha tafiti zinaongeza kuwa watoto wadogo pia ni miongoni mwa waathirika wa ugonjwa wa moyo, wanaoupata kutokana na kurithi kutoka kwa wazazi wao.
    Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam  na Msemaji Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Bw. Maulid Kikondo wakati wa maadhimisho ya  siku ya moyo duniani ambapo kitaifa ilifanyika katika taasisi hiyo.
    Kikondo alisema kuwa katika kuadhimisha siku hiyo Taasisi hiyo imeamua  kupima wagonjwa wa moyo bure ili kuwasaidia wananchi kuweza kufahamu njia bora za kuweka kukabiliana na magonjwa hayo.
    Kikondo alisema kuwa wazee na watoto hupata maradhi ya moyo kwa wingi nchini kutokana kula vyakula visivyo na mpangilio pamoja na kukosa kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
    “Ugonjwa wa moyo huwapata zaidi watoto kutokana kwa kurithi au kutopata mlo ulio bora na mpangilio wakati wazee hupata ugonjwa huu kutokana na msongo wa mawazo pamoja na kutofanya mazoezi mara kwa mara hivyo kupelekea kupata presha na mwisho wake ni ugonjwa wa moyo” alisema Kikondo.
    Aidha Kikondo alisema kuwa wagonjwa wa moyo wanaopatikana kwa siku ni kuanzia wagonjwa 200 na kuendelea kiasi ambacho ni hatari kwa maendeleo ya nchi hasa kwa taifa linaloelekea katika uchumi wa kati.
    Kwa upande wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Delilah Kimambo imesema kuwa inasadikika duniani kote kati ya watu milioni 17.3 hupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa moyo.
    Siku ya Moyo Duniani huadhimishwa Septemba 29 kila mwaka ili kuhamasisha watu kuhusu afya ya Moyo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “YAPE NGUVU MAISHA YAKO”

    No comments:

    Post a Comment