Na Masanja Mabula –Pemba
JUMLA ya magunia 21 ya karafuu kavu na makonyo yamekamatwa na askari wa operesheni ya kuzuia magendo ya karafuu inayoendeshwa na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kisiwani Pemba vikiwa tayari kusafirishwa kupelekwa nje ya nchi kwa njia ya magendo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Operesheni hiyo , Luteni Kanali Jabir Hamza kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) amesema karafuu hizo zimekamatwa Shehia ya Tondooni Wilaya ya Micheweni wakati askari wakiwa katika doria za kawaida.
Amesema kuwa kati magunia hayo , 18 yalikuwa na karafuu kavu wakati matatu pamoja na kipeto kimoja yalikuwa na makonyo .
Luteni Jabir ameeleza kuwa alfajiri ya Semtemba 3, mwaka huu majira ya 10:00 katika ufukwe wa bahari ya Tondooni askari hao walizikamata karafuu pamoja na makonyo hayo zikiwa zinasubiri maji ya yajae ili ziweze kusafirishwa.
“Alfajiri ya leo (jana) huko Tondooni Wilaya ya Micheweni vijana wetu wakiwa katika doria wamefanikiwa kuzima jaribio la kutaka kusafirisha karafuu hizo kwenda nje nchi, na operesheni hii itakuwa ni endelevu” alifahamisha luteni Jabir
Kwa upande wake Kamanda wa KMKM Kamandi ya Pemba Khamis Taji Khamis ameeleza kuwa kikosi chake kitazianika na kuzitenganisha karafuu kavu na makonyo na baadae kuzipeleka Shirika la Biahara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) kwa ajili ya kuuzwa.
“Kwa sasa karafuu pamoja na makonyo hayo yapo chini ya uanglizi wa kikosi cha KMKM Wete , tutazianika na baada ya kukauka tutazikadhiwa uongozi wa ZSTC kwa hatua zaidi” Alifafanua Kamanda Taji.
Nae Kamanda wa Operesheni wa kikosi cha KMKM Pemba Hussein Mohammed Seif amesema kuwa wafanyabiashara wa magendo wamekuwa wakiikosesha Serikali mapato muhimu kwa ajili huduma za kijamii na maendeleo .
Aidha Kamanda Hussein amesisitiza kuwa Serikali haitokua tayari kuona biashara ya magendo inaendelea kufanyika kwani inawanufaisha wachache , huku jamii inakosa fedha kwa ajili ya kusaidia kupatikana huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya , maji barabara na elimu .
Amewataka wafanyabiashara hao kuacha kuichafua sifa ya karafuu ya Zanzibar kwa kuzichanganya na makonyo pindi wanapoenda kuziuzaili kulinda hadhi ya karafuu ya Zanzibar katika masoko ya nje.
Mbali na kukamatwa kwa karafuu hizo hakuna mtu au chombo kinachohusishwa na usafirishaji huo wa na kuwataka wananchi kushirikiaa na vikosi kwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitawezesha kukamatwa kwa wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi kwa kusafirisha karafuu nje ya nchi
No comments:
Post a Comment