• Breaking News

    Friday, 2 September 2016

    CUF Waondolewa Kupisha Mkutano wa Rais Magufuli Pemba



    Jeshi la Polisi Wilaya ya Chakechake, Pemba limezuia kufanyika mkutano na vyombo vya habari wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliokuwa umepangwa kufanyika leo wilayani humo, kupisha ziara ya Rais John Magufuli itakayoanza leo.

    Rais Magufuli anatarajia kuanza leo ziara yake ya kwanza visiwani humo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM. 

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Ikulu, Rais Magufuli atazulu Pemba leo na kesho atakuwa Unguja.

    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani Mohamed Shekhani amesema kuwa zuio hilo la mkutano wa CUF ni kwa sababu eneo wanalotarajia kutumia liko jirani na eneo la uwanja atakaokuwa akihutubia Rais Magufuli.

    Hata hivyo, Katibu wa CUF wilaya ya Chake Chake, Saleh Nassor Juma alilalamikia maamuzi hayo ya Jeshi la Polisi kwa madai kuwa wao walitaka kufanya mkutano na vyombo vya habari na sio mkutano wa hadhara. Alisema kuwa tayari walishawaeleza Idara ya Habari Maelezo  na waliridhia.

    Alisema mkutano huo na waandishi wa habari ulilenga katika kutoa tamko lao kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu la chama hicho kumsimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na viongozi wengine 10.

    “Niliwakatalia kwa hoja kwamba mkutano na waandishi wa habari ni haki yetu ya kikatiba na tulikwishawataarifu watu wa Idara ya Habari Maelezo juu ya kikao hicho halali ambacho wao pamoja na waandishi wa habari walithibitisha kuwa watahudhuria,” alisema Nassor.

    Idara ya Habari Maelezo ilithibitisha kuwa walikubali kufanyika kwa mkutano huo wa CUF na vyombo vya habari lakini baadae walipokea taarifa ya kuahirisha kupisha ugeni wa Rais Magufuli.

    No comments:

    Post a Comment