• Breaking News

    Thursday, 1 September 2016

    Cheyo: Rais Magufuli ni Rais aliyesubiriwa tangu kuanza kwa uhuru


    SeeBait

    Na: Lilian Lundo-Maelezo
    Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais aliyesubiriwa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa Uhuru.

    Cheyo ameyasema hayo alipokuwa akielezea juu ya utendaji wa Rais Magufuli tangu ameingia madarakani Novemba, 2015.

    “Utendaji wa Rais Magufuli umewashtusha watu wengi kwani hawakutegemea kwa muda mfupi aliokuwa madarakani kama angeweza kuchukua hatua kubwa kama vile kupambana na mafisadi, jambo ambalo limekuwa likiongelewa na viongozi waliopita lakini kulikuwa hakuna matunda ya moja kwa moja,” alifafanua Cheyo.

    Ameendelea kwa kusema kuwa Rais Magufuli amekuwa na adhima ya kupambana na Mafisadi na kutatua kero za Taifa tangu akiwa kwenye kampeni huku akisimamia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

    Vile vile Cheyo amesema kuwa kero ambazo amekuwa akizitatua Rais Magufuli zikiwemo ufisadi, uchumi tegemezi, mapato madogo na ukosefu wa vifaa mahospitalini ni kero ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na kambi ya upinzani kwa muda mrefu.

    Hivyo kuingia kwa Rais Magufuli madarakani kumeleta utatuzi mkubwa kwa kero hizo ambazo zimekosa utatuzi kwa muda mrefu kutokana na viongozi waliopita kutozichukulia uzito mfano Rais Magufuli alivyoweza kutatua tatizo la vitanda hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kipindi kifupi ambapo hivi sasa hakuna mgonjwa anayelala nchini katika hospitali hiyo.

    Akielezea suala la ufisadi nchini, Cheyo amesema kuwa ufisadi ni ugonjwa wa muda mrefu ambao umepoteza fedha nyingi za nchi kutokana na mikataba mibovu iliyokuwa ikisainiwa na viongozi wa juu.

    Aidha amempongeza Mhe. Rais kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuona tatizo hilo lishughulikiwe kisheria na kwa njia maalum ili kukomesha ufisadi nchini.

    Cheyo amewataka watanzania kugeuza mawazo yao na kuchukia rushwa kwa kukataa kupokea na kutoa rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na inarudisha nyuma maendeleo 

    No comments:

    Post a Comment