Na Musa Mwakisu.
Uhusiano wa meneja wa Man United na Depay unampa nafasi kubwa zaidi ya washindani wake Liverpool na Bayern Munich Manchester United wana nafasi kubwa katika mbio za kumuwania saini ya Memphis Depay anayefananishwa na ‘Cristiano Ronaldo’ kwa sababu ya Louis van Gaal. Mkongwe wa soka la Uholanzi Ronald de Boer anadai kuwa uhusiano wa meneja wa United na winga wa PSV Eindhoven, Depay, unamuweka kwenye nafasi ya mbele ya kumsajili mmoja wa wachezaji wanaowindwa sana msimu huu wa majira ya joto barani Ulaya. Van Gaal alimtaja mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 katika kikosi chake cha Uholanzi kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia la msimu uliopita. De Boer anaamini kuwa uhusiano wao wa pamoja wakati wa kombe la Dunia nchini Brazil utaipa United nafasi dhidi ya washindani wake kama vile Liverpool na Bayern Munich kwa ajili ya kunyakua mchezaji huyo mwenye thamani ya yuro milioni 25. “Sitaki kusema ni klabu ipi inamfaa zaidi,” alisema nyota huyo wa zamani wa Ajax. “Lakini akienda United anajua kuwa kule kuna kocha Mholanzi, Van Gaal, ambaye anamjua tokea mashindano ya Kombe la Dunia. “Hiyo ni fursa. Ni mmoja wa vipaji vikubwa kabisa barani Uaya- ana kila kitu.” PSV imethibitisha kuwa United imeshaelezea kuwa inataka kumnyakua mchezaji huyo. Mabingwa hao wa Uholanzi wamekubali pia kuwa watamuuza Depay wakati wa majira ya joto, baada ya ubora
aliouonesha msimu huu. Magoli yake 20 yalifanikisha PSV kutwaa ubingwa na yamemfanya kuwindwa na baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya. De Boer anaamini wazi kuwa atafanya vizuri akiwa United kutokana na kufanana na nyota wa zamani wa United. “Ana ufundi unaolinganishwa na Cristiano Ronaldo,” aliongeza. “Ana nguvu, ana ufundi, ana kipawa, ana kasi sana, ana rikodi nzuri ya ufungaji, anaweza kupiga mashuti ya mbali – ana kila kitu. “Kwangu mimi, bila shaka ni mmoja wa vipaji vikubwa kabisa tulivyonavyo.” Depay ndiye mfungaji kinara wa Eredivisie. Van Gaal anatarajia kukabidhiwa kiasi cha £150m ili kuimarisha kikosi chake. Mbali na Depay, United pia wameonesha kuwahitaji wachezaji wengine kama Gareth Bale, Mats Hummels, Kevin Strootman, Danny Ings na Nathaniel Clyne. Kocha wa PSV Phillip Cocu amekiri kuwa Depay ataondoka mwishoni mwa msimu huu. “Ni bahati mbaya, lakini kwa upande mwingine kama klabu tunapaswa kujivunia kwa sababu sisi ndio tumemfunda,” alisema. “Kwa upande mwingine ni wazi kuwa yuko tayari kwa hatua inayofuata. Nadhani ataondoka PSV baada ya msimu huu.” Depay ameashiria kuwa ataikaribisha hatua yoyote ya kuelekea United na ameonesha hamu ya kwenda Old Trafford. Wakati De Boer akimuona kuwa ni mchezaji anayefanana na Ronaldo, Cocu amemfananisha na Arjen Robben ambaye mwanzo alikuwa akiwindwa na Van Gaal.
No comments:
Post a Comment